Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa mawili ndio muarobaini kwa Israel na Palestina- Guterres

Mataifa mawili ndio muarobaini kwa Israel na Palestina- Guterres

Pakua

Katibu Mkuu  wa Umoja wa mataifa António Guterres akiwa katika ziara ya siku tatu  huko Mashariki ya Kati amesema ni muhimu kuanzisha  upya mchakato wa amani unaoaminika.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa pamoja na Waziri Mkuu wa Palestina, Rami Hamdallah Bwana Guterres amesema mchakato huo kati ya Israel na Palestina utasaka ufumbuzi kuhusu suluhu ya kuwepo kwa mataifa mawili.

Baadaye akiwa Ramallah Katibu Mkuu amewaambia waandishi wa habari  kwamba hakuna mpango mbadala kuhusu upatikanaji wa amani kati ya Israeli na Palestina, isipokuwa pande mbili hizo kukaa pamoja na kutafuta suluisho.

Amesema upanuzi wa makazi ya Israeli kwenye eneo inalokalia la wapalestina ni kinyume cha sheria ya kimataifa .

(Sauti ya Guterres)

"Ni imani yangu kwamba ni muhimu kuanzisha upya mchakato wa kisiasa wenye kuaminika kwa lengo la  suluhisho la serikali mbili. Pia ni muhimu kuunda mfumo wenye lengo la kuboresha hali ya kiuchumi  unaoweza kuinua maisha ya wapalestina.”

Bw. Guterres amesisitiza kwamba  pamoja na msaada wa Umoja wa Mataifa kwa  wapalestina , Rais Mahmoud Abbas ana wajibu wa  kuunda serikali  ya umoja  ikishirikisha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ukanda wa Gaza, ambako bado wako chini ya udhibiti wa kikundi cha Hamas.

Photo Credit
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres awasili kwenye Kituo cha waathirika wa vurugu huko Ramallah, Palestina. Picha: Picha ya UN / Ahed Izhiman