Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 200 kusaidia Yemen kukabili Kipindupindu

Dola milioni 200 kusaidia Yemen kukabili Kipindupindu

Pakua

Benki ya Dunia imetangaza mkopo nafuu wa dola milioni 200 kwa Yemen ili iweze kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Kristalina Georgieva, ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo amesema fedha hizo zitasaidia kuimarisha mifumo ya maji, afya na majitaka nchini humo na pia kuepusha milipuko ya ugonjwa huo siku za usoni.

Mathalani kupitia mkopo huo wenye masharti nafuu, wahudumu wa afya 7,500 watapatiwa mafunzo ili kuimarisha uwezo wao wa kutibu wagonjwa, halikadhalika uwekaji wa vidonge vya kutakatisha maji na pia kuendesha kampeni za kuhamasisha afya ya umma.

Fedha pia zitatumika kwenye utoaji chanjo dhidi ya kipindupindu wakati huu ambapo zaidi ya wananchi nusu milioni wameambukizwa ugonjwa huo katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.

Bi. Georgieva amesema ni muhimu zaidi hivi sasa kwa Benki ya Dunia kuwekeza katika miundombinu ya afya na maji nchini humo ili kuhakikisha hata amani itakaporejea, wananchi wako tayari kushiriki kikamilifu kujenga nchi yao.

Photo Credit
Mama na mwanae aliyelazwa katika kituo cha afya kufuatia maradhi ya kipindupindu. Picha: UNICEF