IOM yazindua mradi wa kuchagiza ajira ya vijana Burkina Faso
Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM leo limesema limezindua mradi mpya unaoshughulika na uhusiano kati ya vijana, ajira na uhamiaji katikati na Mashariki Burkina Faso.
Mradi huo unalenga kukuza uajiri wa vijana na ujasiriamali ili kupunguza hatari ya uhamiaji katika kanda hiyo Burkina Faso, kama ilivyo nchi zingine za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inashuhudia ongezeko la uhamiaji kutokana na ukosefu wa ajira na kutokuwepo fursa za vijana kujipatia kipato .
Kwa mujibu wa IOM vijana ndio wahanga wakubwa wa ukosefu wa ajira nchini humo kutokana na vigezo hafifu vya kuweza kuajiriwa ambapo asilimia 66.7 ya vijana nchini Burkina Fasso hawajapata mafunzo ya aina yoyote na wanakabiliwa na ugumu wa kupata fursa za kujikimu na hivyo kutumbukia katika hatari ya uhamiaji.
Mradi huo wa miaka mitatu unachangia katika maendeleo ya kiuchumi nchini humo na kukabiliana na tatizo la uhamiaji kwa kuelimisha vijana kuhusu hatari za uhamiaji katika kanda hiyo.