Alison Smale kuwa mkuu mpya wa mawasiliano ya kimataifa UM

Alison Smale kuwa mkuu mpya wa mawasiliano ya kimataifa UM

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  António Guterres amemteua Alison Smale wa Uingereza kuwa msaidizi wa Katibu mkuu kuhusu mawasiliano ya kimataifa , kwenye idara ya habari kwa umma ya Umoja wa Mataifa (DPI).

Bi Smale anakuwa mrithi wa  Cristina Gallach wa Hispania ambaye Katibu Mkuu amemshukuru kwa utendaji wake na huduma aliyoitoa kwa Umoja wa Mataifa. Katibu Mkuu pia amemshukuru Maher Nasser ambaye amekuwa akikaimu katika wadhifa huo.

Smale ambaye amekuwa mkuu wa ofisi ya The New York Times mjini Berlin tangu mwaka 2013 anakuja na ujuzi wa takribani miaka 40 katika tasnia ya uandishi wa habari alioupata katika nyanja ya kimataifa ambayo inajumuisha kushika nafasi mbalimbali za juu katika tasnia hiyo.

Ana rekodi nzuri kama ripota, mhariri, na kiongozi wa ngazi ya juu, ikiwemo kuteuliwa kuwa mhariri mtendaji wa gazeti la Herald Tribune (IHT) Paris mwaka 2008, ambapo alikuwa mwanamke wa kwanza na pekee kuwahi kushika wadhifa huo.

Bi Smale alikwenda Herald Tribune mwaka 2004 kama mhariri mkuu akitokea New York Times, ambako alikuwa mhariri mwandamizi wa habari za kigeni tangu kwama 2002.

Alijiunga na New York Times kama mhariri wa habari za kigeni za mwishoni mwa wiki mwaka 1998. Na kabla ya hapo Bi smale aliwahi kuwa ripota wa United Press International na mkuu wa kituo cha ulaya ya Kati na Mashariki cha The Associated Press (AP) mjini Vienna mwaka 1986-1998. Pia alikuwa mwandishi wao mjini Moscow na Bonn 1983-1986, na 1978-1983.

Bi Smale alisoma Bristol, Munich na chuo kikuu cha Stanford. Ana shahada ya sayansi ya jamii katika masuala ya Ujerumani na siasa , na ana stashahada ya uzamili ya masuala ya uandishi wa habari.

Mwaka 2009 alitunukiwa stashahada ya uzamivu (PHD) ya sheria kutoka chuo kikuu cha Bristol.

Photo Credit