Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi wa kesho Kenya uwe wa salama na haki:OHCHR

Uchaguzi wa kesho Kenya uwe wa salama na haki:OHCHR

Pakua

Wataalamu huru watatu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameisihi mamlaka nchini Kenya kuhakikisha hali ya utulivu na uchaguzi salama, pamoja na mchakato wa uchaguzi uliowazi na wa haki.

Ili kutorejelea hali ya machafuko na ukatili wa mwaka 2007, wataalamu hao wametoa wito kwa serikali ya nchi hiyo kuwahimiza wadau wote katika uchaguzi kuhakikisha kiwango cha juu zaidi cha utendaji kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa Jumanne.

Wamekumbusha kuwa kuheshimu haki na uhuru wa msingi wa watu - ikiwa ni pamoja na haki ya kupiga kura, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika ni misingi ya uchaguzi huru na wa haki na ushiriki wa umma.

Wamesema Kenya imepiga hatua kubwa tangu uchaguzi wa mwaka 2007 katika kuimarisha demokraisia, haki za binadamu na sheria, vile vile imeweka umuhimu katika kuleta utengamano baina ya makundi ya uhasama katika uchaguzi, lakini matukio ya hivi karibuni ya migogoro ya kisiasa, hotuba za chuki na mvutano uliopo, ni muhimu kusisitiza kwa wale wote wanaohusika kuhakikisha mwenendo wa amani wakati na baada ya uchaguzi.

Wamekumbusha jukumu la vikosi vya usalama katika uwezeshaji wa maandamano ya amani, na kuzingatia kanuni za tahadhari pindi maandamano yanapogeuka vurugu.

Photo Credit
UN Photo/Albert Gonzalez Farran