Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMA yalaani shambulio kwenye ubalozi wa Iraq , Kabul

UNAMA yalaani shambulio kwenye ubalozi wa Iraq , Kabul

Pakua

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA, umelaani vikali shambulio la leo dhidi ya ubalozi wa Iraq mjini Kabul.

Shambulio hilo lililotokea katika makazi ya watu katikati mwa Kabul lilidumu kwa saa tano na lilihusisha watu kadhaa wenye silaha ambao waliwauwa raia wawili wa Afghanistan waliokuwa wakifanya kazi katika ubalozi huo na kumjeruhi afisa wa polisi kabla ya washambuliaji hao kuuawa na vikosi vya Afghanistan.

Kundi la IS kutoka jimbo la Khorasani limedai kuhusika na shambulio hilo. UNAMA inasema hili ni shambulio lingine linaloonekana kulenga jumuiya ya kimataifa lakini mwisho wa siku raia wa Afghanistan ndio wanaoonekana kubeba gharama kubwa ya maisha yao.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Tadamichi Yamamoto, shambulio la leo linaonyesha kutojali kabisa uhai wa binadamu na sheria za kimataifa zilizotengwa kuwalinda wanadiplomasia.

Hata hivyo amelipongeza jeshi la usalama la Afghanistan kwa hatua madhubuti walizochukua wakati wa shambulio hilo na kusema zimesaidia kuokoa maisha ya wengi.

Ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kuwatakia nafuu ya haraka majeruhi.

Photo Credit