Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zimeweka sera thabiti kulinda watu dhidi ya matumizi ya tumbaku-Ripoti, WHO

Nchi zimeweka sera thabiti kulinda watu dhidi ya matumizi ya tumbaku-Ripoti, WHO

Pakua

Ripoti ya Shirika la afya ulimwenguni, WHO kuhusu janga la tumbaku 2017, imebaini kuwa nchi nyingi zimeweka sera za kukabiliana na matumizi ya tumbaku iwe ni maandishi yanyopatikana katika makasha ya bidhaa hizo, marufuku ya matangazo au udhibiti wa maeneo ya kuvuta sigara.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo watu bilioni 4.7 ambao ni asilimia 63 ya idadi ya watu wote ulimwenguni wanalindwa na aina moja au zaidi ya udhibiti wa matumizi ya tumbaku, hali ambayo imeongezeka mara nne ikilinganishwa na ilivyokuwa 2007 wakati watu bilioni moja tu au asilimia 15 ya watu walikuwa na sheria zinazowalinda dhidi ya bidhaa hizo.

Akiwasilisha ripoti hiyo mkurugenzi mkuu wa WHO, Dr Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema licha ya hatua zilizopigwa sekta ya tumbaku inaendelea kukandamiza juhudi za serikali za kuwekeza kikamilifu katika mikakati ya kuokoa maisha na yenye bei nafuu.

Dr Tedros ameongeza kuwa kwa kufanya kazi pamoja, nchi zinaweza kuzuia vifo vya mamilioni ya watu ambao wanafariki dunia kwa sababu ya magonjwa yanayotokana na matumizi ya tumbaku na kuokoa mabilioni ya dola kila mwaka yanayotumika kusaka huduma za afya na kudumaza nguvu kazi.

Matumizi ya tumbaku yanaweka watu katika hatari ya magonjwa yasiyoambukizwa ambayo yanasababisha vifo vya watu milioni 40 kila mwaka ambayo ni sawa na asilimia 70 kote ulimwenguni, wakiwemo watu milioni 15 walio na umri kati ya 30-69, huku takriban vifo asilimia 80 vikitokea katika nchi maskini na zile za kipato cha wastani.

Photo Credit
Huyu ni mjenzi anachukua muda kuvuta sigara nchini Timor Leste.(Picha:Benki ya dunia/Alex Baluyut)