Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujuzi wa kiuchumi wa miaka 70 ni somo kwa SDG's

Ujuzi wa kiuchumi wa miaka 70 ni somo kwa SDG's

Pakua

Ripoti ya Kimataifa ya Kiuchumi na Kijamii ya 2017 iliyotolewa leo na idara ya uchumi na masuala ya kijamii ya Umoja wa Mataifa DESA , imeweka bayana kuwa uchambuzi bado ni muhimu katika kuongoza mataifa wakati huu ambapo dunia inapitia hali ngumu ya kiuchumi na pia katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030.

Tathmini ya ripoti hiyo imeonyesha kuwa nchi nyingi zimetumia njia tofauti za maendeleo katika kipindi hiki ambacho ulimwengu umeshuhudia kukua kwa haraka zaidi kwa pato la kimataifa na biashara kuliko kipindi kingine chochote katika historia ya binadamu, na kwamba katika miaka sabini ya uchunguzi wa kina wa uchumi uliofanywa na Umoja wa Mataifa umegundua kwamba uhuru wa biashara, maendeleo rafiki, na ushauri maalumu wa nchi kuhusu utafiti huo umethibitisha kuwa ni sahihi na tabirifu.

Hata hivyo, uchunguzi wa ripoti hiyo pia umebaini kwamba baada ya hali ya wasiwasi ya kifedha ya mwaka 2008, kufikia SDG's inaweza kuwa vigumu. Diana Alarcón ni Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji wa Uchumi katika Idara ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi na Jamii ,DESA.

(Sauti ya Diana)

"Hali ya sasa hivi ulimwenguni haiweki mazingira mazuri ya utekelezaji wa ajenda kama ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, na ushirikiano bora wa kimataifa utahitajika zaidi kuweka mazingira mazuri ya maendeleo."

Akizungumzia kuhusu ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema pamoja na mabadiliko makubwa kimaendeleo ulimwenguni, changamoto zinazokumba jumuiya za kimataifa hivi sasa na siku za nyuma zinalingana, akibainisha kuwa ajenda ya 2030 ni muhimu kimaadili na kiuchumi na ni fursa ya ajabu, na hivyo utafiti wa ripoti hiyo wenye mapitio ya miaka 70 unatoa fundisho na mwelekeo wa mbele katika kufanikisha ajenda hiyo.

Photo Credit