Skip to main content

Uaminifu ni muhimu sana katika kuwalinda watoto walio pekee yao-UM

Uaminifu ni muhimu sana katika kuwalinda watoto walio pekee yao-UM

Pakua

Mkakati kabambe umezinduliwa leo kwa ajili ya kuwalinda watoto wakimbizi na wahamiaji dhidi ya ghasia na ukatili wakati wanapoelekea na kusafiri ndani ya bara Ulaya.

Mkakati huo uliotangazwa Jumatatu na Umoja wa Mataifa upo katika waraka uiitwao “Ramani ya mwelekeo” ambayo ni kazi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, shirika la kuhudumia watoto UNICEF na kamati ya kimataifa ya uokozi (IRC).

Miongoni mwa mapendekezo yaliyopo katika waraka huo ni pamoja na kuhakikisha wasaidizi wanaaminiwa na watoto hao ambao mara nyingi hawana mtu wa kumtegemea na kusalia kutegemea huruma ya wasafirishaji haramu. Diane Goodman ni afisa wa UNHCR.

(Sauti ya Diane)

“Watoto wanaweza kukimbia kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita, ghasia, mauaji na kwa sababu zingine pia na ndio sababu ni muhimu kuwa na uhusiano wa kuaminiana kwanza, kwa sababu kama hauna huo huwezi kushirikiana nao na kuwasaidia kuamua kipi ni cha faida kwao,”

Ameongeza kuwa UNHCR inatoa wito wa mshikamano na nchi ambazo zimepokea wimbi kubwa la watoto wasio na mlezi au mzazi.

(Sauti ya Diane)

“Kwa ujumla tunatoa wito wa mshikamano, kuwahamisha watoto hawa ni kipengee muhimu, hadi sasa hakuna watoto wengi walioweza kuhamishwa kutoka Italia kwenda nchi zingine, lakini tunatoa wito kwa nchi zote ambako watoto wako, kuwapa huduma inayostahili , kuwa marafiki wa watoto hao na kurahisisha upatikanaji wao ili watoto waelewe hali halisi na pia kuwatafutia suluhu ya haraka ambayo ni ya manufaa kwao.”

Photo Credit
Watoto wacheza katika kambi ya Kara Tepe katika vitongonji vya Mytilini, Lesvos, Ugiriki.(Picha: UNICEF/UN057951/Gilbertson VII)