Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kimbunga Mora chasambaratisha kambi za wakimbizi wa Rohingya

Kimbunga Mora chasambaratisha kambi za wakimbizi wa Rohingya

Pakua

Kimbunga Mora kilichokuja na upepo mkali wa kilometa 117 kwa saa, kimepiga Kusini-Mashariki mwa Bangladesh Jumanne, na kuathiri mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Rohingya katika kambi za Kutupalong na Nayapara, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR.

Limesema kimbunga Mora kimeharibu maelfu ya nyumba za wakazi wa eneo hilo, na hivi sasa wakimbizi zaidi ya 20 waliojeruhiwa katika kambi hizo wamepata matibabu, na wameweza kuepukana na maafa makubwa zaidi kutokana na ushirikiano wake na serikali za mitaa katika kuwandaa wakimbizi mapema na kimbunga hicho.

Kabla ya Mora, UNHCR iliweka wafanyakazi wake tayari kutoa usaidizi, kuandaa na kuwahamishia watu kwenye maeneo thabiti zaidi, pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa na wajawazito, lakini ukosefu wa umeme umesalia changamoto kwa wakimbizi kupata maji safi na maeneo ya kujisafi.

UNHCR wa kushirikiana na wadau wengine wa Umoja wa Mataifa wanatoa usaidizi wa haraka kwa waathirika, pamoja na kufanya tathmini ya hali halisi ya mahitaji na uharibifu.

Photo Credit
Picha:ILO