Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi wa WHO Afrika aenda DRC kujadili kukabili Ebola:

Mkurugenzi wa WHO Afrika aenda DRC kujadili kukabili Ebola:

Pakua

Mkurugenzi wa kanda ya Afrika wa shirika la afya duniani WHO, Dr. Matshidiso Moeti leo Jumamosi amezuru Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC  kujadili na uongozi wa nchi hiyo na wadau wengine njia muafaka na za haraka za kudhibiti kuenea kwa mlipuko wa Ebola nchini humo.

Ziara hiyo inafuatia taarifa ya serikali ya DRC kwa shirika la WHO kuhusu  mlipuko wa virusi vya homa ya  Ebola katika kituo cha afya cha Likati jimbo la Bas Uele kaskazini mwa nchi . Shirika hilo linasema hadi leo Jumamosi Mei 13 kuna visa 11 vinavyoshukiwa, na vifo vitatu vimeripotiwa.

Akizungumza katika mkutano mjini Kinshasa , Dr Moeti amesema yuko hapo kuihakikishia serikali ya DRC kwamba kwa ushirikiano na mfumo wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine watafanya kazi pamoja kukabiliana na mlipuko huo.

WHO tayari imeshaandaa  timu ya watalamu ya kupelekwa huko na iko tayari kusimamia na kutoa usaidizi wa kitaalamu unaohitajika kuratibu juhudi za kukabili mlipuko huo.

Dr. Moeti ameuchagiza umma kushirikiana na mamlaka za afya na kuchukua hatua muhimu zinazohitajika kujikinga kiafya.

Tarehe 10 Mei timu iliyoongozwa na wizara ya afya ya DRC na kusaidiwa na WHO na wadau wengine ilipelekwa Likati  jimbo la Bas-Ulele  ili kufanya uchunguzi wa kina wa mlipuko huo. Kisa cha kwanza kilitokea Aprili 22 ambapo mwanaume mwenye miaka 45 alikuwa mgonjwa akasafirishwa kwa teksi kwenda hospitali na aliaga dunia walipowasili tu.

Huu ni mlipuko wa 8 wa Ebola DRC tangu ugonjwa huo ulipobainika nchini humo 1976.

Photo Credit