Wayazid 36 wanasuliwa kutoka kwa ISIS nchini Iraq

Wayazid 36 wanasuliwa kutoka kwa ISIS nchini Iraq

Pakua

Huko nchini Iraq, kundi la wayazid 36 wakiwemo wanawake, wanaume na watoto wameokolewa baada ya kuwa wanashikiliwa utumwani na kundi la magaidi la ISIS au Da’esh kwa takribani miaka mitatu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuwa hivi sasa wayazid hao ambao ni raia wa Iraq wanapatiwa usaidizi maalum kwenye kituo kilichoandaliwa na shirika la mpango wa idadi la umoja huo, UNFPA kwa ufadhili wa Uholanzi.

Misaada hiyo ni pamoja na nguo, malazi na usaidizi wa kisaikolojia kutokana na madhila waliyopitia ambapo amemnukuu mratibu wa usaidizi wa kibinadamu nchini Iraq Lise Grande akisema kuwa..

 (Sauti ya Dujarric)

“Kile ambacho wanawake hawa wamepitia hakiwezi kufikirika na kwamba Umoja wa Mataifa kupitia UNFPA inafanya kile linalowezekana kuwapatia  wanawake na wasichana hao msaada maalum wa kimatibabu na kisaiokolojia ambao wanahitaji.”

Yakadiriwa kuwa wanawake na wasichana 1,500 bado wanashikiliwa na Da’esh na yawezekana wanakabiliwa na ukatili wa kingono.

Photo Credit
Akiwa amembeba mtoto mwenye umri wa siku 13, mwanamke huyu ni mmoja wa raia wa Iraq wa kabila la Yazidi ambao wamekimbia kutoka mlima wa Sinjar hadi Syria na hatimaye kuweza kuingia upya Iraq ili kukwepa madhila. (PICHA:Maktaba/UNICEF/Wathiq Khuzaie)