Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuzibe pengo la waathirika wa malaria-WHO

Tuzibe pengo la waathirika wa malaria-WHO

Pakua

Katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Malaria ulimwenguni inayofanyika kila mwaka Aprili 25 , Shirika la Afya Duniani WHO limetoa wito Jumatatu jijini Nairobi, Kenya wa kuongeza juhudi za kuzuia Malaria ili kuokoa maisha hususan kusini mwa jangwa la Sahara, ambako kunabeba mzigo mkubwa wa ugonjwa huo kwa asilimia 90% ya visa vyote vya malaria duniani.

Katika ripoti yake iitwayo “Kuzuia Malaria kunawezekana: Hebu Tuzibe Pengo",WHO inasema tangu mwaka 2001, imefanikiwa kutibu visa milioni 663, matumizi ya vyandarua vya mbu ikiwa ni mojawapo ya sababu kuu ya mafanikio hayo. Vile vile imependekeza kupuliza dawa za kuua wadudu ukutani, pamoja na dawa za kuzuia malaria kwa vikundi vilivyohatarini zaidi kama kina mama wajawazito, watoto wachanga na watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.

Hivyo imetoa wito kwa wahusika hususan barani Afrika, kuhakikisha wale wanaoathirika zaidi kupata huduma hizo, kwani mwaka 2015 asilimia 43 ya wakazi wa kusini mwa jangwa la sahara hawajapata vyandarua wala vifaa vya kuwakinga na ugonjwa huo.

Photo Credit
Msichana akiwa ndani ya neti Magharibi mwa Bengal, India.(Picha: WHO/Joydeep Mukherjee)