Skip to main content

Zahma inayoighubika Mashariki ya Kati yatishia amani ya kimataifa-UM

Zahma inayoighubika Mashariki ya Kati yatishia amani ya kimataifa-UM

Pakua

Zahma kubwa imeighubika Mashariki ya Kati na inaendelea kutishia amani na usalama wa kimataifa amesema mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati.

Nickolay Mladenov ametoa kauli hiyo Alhamisi wakati wa mjadala wa baraza la usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati.

Katika nchi nyingi amesema , jamii zimeathirika kutokana na machafuko ya kikabila na misingi ya dini, na kuwatawanya mamilioni ya watu katika kile Umoja wa mataifa unachokieleza kuwa ni mgogoro mkubwa kabisa wa wakimbizi tangu vita ya pili ya dunia.

Mladenov aliyeanza hotuba yake kwa kuwakumbuka wote waliopoteza maisha katika ghasia kwenye ukanda huo, ametoa wito kwa viongozi wa kimataifa kuushinda ugaidi na kusaidia kutatua kitendawili cha kisiasa, kiuchumi na majeshi ya nje ambavyo vinahanikiza mzozo wa Mashariki ya Kati.

Ameeleza hali halisi ikiwemo Israel kuendelea na ujenzi wa makazi ya Walowezi, mtafaruku wa umeme Gaza na kuimarika kwa kundi la wanamgambo la Hamas

(SAUTI YA MLADENOV)

"Hamasa inaendelea kujiimarisha Gaza kwa kuanzisha kamati ambayo inaonekana na wengi kama upinzani wa moja kwa moja dhidi ya serikali halali ya Palestina.Kufuatia kuuawa kwa mmoja wa wanamgambo wake imeweka vikwazo vya muda vikiwazuia Wapalestina na raia wa kigeni kuondoka na imepiga marufuku uvuvi kwa wiki mbili.Aprili 6 Wapalestina watatu walinyongwa na Hamas katika ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Vitendo hivyo vimelaaniwa na Katibu Mkuu na nina hofia kwamba mauaji zaidi yanatarajiwa Gaza."

Amezungumzia pia mzigo mkubwa wa wakimbizi wa Syria katika nchi za ukanda huo akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia zaidi, na pia madhila ya kutawanywa kwa maelfu ya watu Iraq kufuatia operesheni za ukombozi wa Mosoul.

Photo Credit
Mratibu maalumu wa UM kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov. (Picha:UM/Eskinder Debebe)