Mwenyekiti wa AU afanya ziara Somalia

Mwenyekiti wa AU afanya ziara Somalia

Pakua

Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika AU, Moussa Faki Mahamat, amefanya ziara rasmi nchini Somalia, ziara inayoelezwa kuwa inalenga kufufua amani na usalama nchini humo.

Taarifa ya AMISOM kuhusu ziara ya kiongozi huyo inaeleza kuwa imekuja wakati muafaka ambapo taifa hilo limefanikisha mchakato wa uchaguzi wa bunge na Rais, na mwanzoni mwa mwezi huu muungano huo umeadhimisha miaka 10 tangu kupelekeka vikosi vyake Somalia.

Bwana Mahamat ametumia ziara hiyo kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoa usaidizi muhimu kwa vikosi vya Somalia ili vitekeleze wajibu wake wa msingi wa kutoa ulinzi kwa watu wa Somalia na kujenga mazingira bora ya maridhiano.

Kadhalika ameunga mkono nia ya Rais wa taifa hilo ya kuhakikisha wapiganaji wa kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab wanaondolewa kabisa nje ya Mogadishu na nchi nzima kwa kuunga mkono vikosi vya Somalia, na adhma yake ya kukabiliana na rushwa na kufanya kila awezalo kuleta ahueni kwa raia wa taifa hilo la pembe ya Afrika ambalo wameteseka kwa muda mrefu kutokana na uakme.

Photo Credit
Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika AU, Moussa Faki Mahamat alipokutana na rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmaajo.(Picha:AMISOM/Omar Abdisalan)