Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Polisi mwanamke apigania haki za wanawake Somalia

Polisi mwanamke apigania haki za wanawake Somalia

Pakua

Mwanamke mmoja ambaye aliishi ukimbizini nchini Kenya, sasa ameamua kurejea nchini mwake Somalia, ambapo licha ya kazi ngumu ya kurejesha amani baada ya mapigano ya miongo miwili sasa, amejitokeza mbele katika kuchangia ujenzi wa sheria nchini humo na kupigania haki za wanawake.

Bi. Amino Hiirey Ali ambaye ni afisa wa jinsia wa jeshi la Polisi la Hiraan katika mji wa Belet Weyne anasema polisi wa mji huo ni rafiki wa wanawake na yeye ni rafiki wa wanawake wa mji huo, na anatumia nafasi hiyo kuhakikisha visa vyote dhidi ya ukiukwaji wa haki za wanawake zinatatuliwa kikamilifu.

Amesema kazi hiyo ambayo aliitamani tangu utotoni sasa ameipata, na anahakikisha anawasaidia wanawake na wasichana ambao wanakabiliwa na ubakaji, ukatili majumbani, na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia, na hadi sasa amefanikiwa kuwatia rumande wahalifu wengi wa ukatili huo na amepata sifa kubwa na imani kwa wanawake wa mji huo.

Mbali na kazi yake, na katika joto kubwa, yeye vile vile hujitolea kutembea mchana kutwa kutoa masomo ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu athari za ukatili dhidi ya wanawake.

Amesema anatambua kuwa bado safari ya kurejesha amani na utulivu nchini humo ni ndefu, lakini ana matumaini makubwa na utawala wa sheria, hususan kuhusu wanawake na wasichana na hiyo ni hatua kubwa tayari.

Photo Credit
Amino Ali Hiirey. Picha:UNSOM