Skip to main content

Kuna hatari ya watu kufa kwa njaa pembe ya Afrika- UNHCR

Kuna hatari ya watu kufa kwa njaa pembe ya Afrika- UNHCR

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema kuna hatari kubwa ya watu kufa kwa njaa huko pembe ya Afrika, Yemen na Nigeria kutokana na ukame ulioathiri nchi nyingi, mizozo huku fedha za usaidizi zikipungua.

UNHCR inasema kutokana na mazingira hayo idadi ya wakimbizi wa ndani na nje inaongezeka ikitolea mfano Sudan ambako wakimbizi wanaokadiriwa kuingia kutoka Sudan Kusini ilikuwa 60,000 lakini inakadiriwa kuongezeka hadi 180,000.

Kama hiyo haitoshi, mgao wa chakula kwa wakimbizi umepunguzwa kwa kati ya asilimia 20 hadi 50 huko Ethiopia, Tanzania na Rwanda, watoto wakiwa hatarini zaidi kukumbwa na utapiamlo.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Adrian)

"Watoto ndio idadi kubwa zaidi ya wakimbizi katika nchi hizi, na kwa kawaida wengi wanahitaji msaada wa chakula kutoka kwa WFP. Bila ufadhili migao ya chakula inapunguzwa."

UNHCR inasema uhaba wa chakula umesababisha utoro wa watoto shuleni ikitolea mfano Kenya ambako watoto 175,000 kwenye maeneo ya ukame wameacha kwenda shule ilhali nchini Ethiopia, shule 600 zimefungwa.

Photo Credit
Wakimbizi pembeni mwa Africa.Picha: UNHCR