Bila ushirikiano wetu hatutatimiza SDG's
Kongamano la mwaka huu la Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC kuhusu Ushirikiano limefanyika leo jijini New York, Marekani kujadili hatua za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
Akihutubia kwa njia ya video katika mkutano huo ulioleta pamoja wadau wa kimataifa, asasi za kiraia na makampuni binafsi, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi. Amina Mohammed amesema, wakati wa kupitisha ajenda ya 2030, mataifa yalijua urefu wa kiwango chake, na vile vile yalifahamu kwamba hayawezi kuzifikia bila ushirikiano jumuishi na thabiti, akiongeza kuwa..
"Kukuza ushirikiano fanisi kutahusisha mkazo zaidi katika ubunifu, athari, uwazi, mshikamano, uwajibikaji na uendelevu. Ni jambo muhimu sana katika juhudi zetu za sasa katika kuwezesha Umoja wa Mataifa kusaidia nchi kutimiza malengo ya 2030 na ahadi za mabadiliko ya tabianchi."
(Sauti ya Thompson)
"Ikiwa tunataka malengo ya maendeleo endelevu yapatikane katika kipindi cha miaka 13, na ikiwa tunataka matumaini yoyote ya mustakabali endelevu kwa ajili yetu wote, ni lazima tuachilie mbali malalamiko ya zamani na wasiwasi, na tuungane pamoja kwa nguvu katika fikra mpya, tushirikiane, tuwekeze kifedha, na kujitolea mashinani".