Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji 655 wafariki wakisaka hifadhi-IOM

Wahamiaji 655 wafariki wakisaka hifadhi-IOM

Pakua

Shirika la kimataifa la wahamiaji IOM linasema wahamiaji na wakimbizi karibu 700 wamefariki katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka huu wa 2017 wakati wa safari za kusaka hifadhi sehemu mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo msemaji wa IOM Joel Millman amesema idadi hiyo hata hivyo bado haijavuka ile ya kipindi cha miezi mitatu ya mwaka jana ambapo wahamiaji na wakimbizi 749 walifariki katika kipindi hicho.

Amesema nchini Libya shirika hilo limeripoti kupatikana kwa masalia ya miili saba katika ufukwe wa bahari hapo jana na kuongeza kuwa taarifa za vifo vya wahamiaji 146 raia wa Gambia hazijathibitishwa baada ya mtoto mwenye umri wa miaka 16 kutoa ushuhuda huo licha ya kwamba alikuwa katika hali ya mstuko.

( Sauti Millman)

‘‘Mnamo Machi 30, IOM imeonyesha picha ya huyu mtoto kwa manusura 140, ambao wamethibitisha kwamba walikuwa katika boti moja na mtoto huyo. Janga hilo halijatokea kama lilivyoripotiwa awali.’’

Kadhalika amesema zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 27,000 wamewasili barani Ulaya kwa njia ya maji katika kipindi cha mwanzo wa mwaka huu wa 2017, asilimia 80 wakiwasili nchini Italia, wengine nchini Hispania na Ugiriki.

Photo Credit
Picha:IOM