Kukaa chumba kimoja hata wakati wa ufunguzi ni dalili njema- Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameeleza kutiwa moyo kufuatia hatua ya wasyria waliokubali mwaliko wa umoja huo katika kufufua majadiliano ya kusaka suluhu mjini Geneva Uswisi, kukaa katika chumba kimoja wakati wa ufunguzi wa mazungumzo hayo siku ya Alhamisi.
Katika taarifa yake kupitia msemajiwa Katibu Mkuu, Guterres amepongeza kazi ya mwakilishi wake maalum katika kutekeleza jukumu lake la kuzileta pande kinzani pamoja na kwa kufufua majadiliano.
Ameshukuru uwepo wa baraza la usalama na kikundi cha kimataifa cha usaidizi kwa Syria, kwa kukaribisha majadiliano na kusisitiza umuhimu wa umoja wa jumuiya ya kimataifa katika kuunga mkono mchakato wa kisiasa wa kusaka suluhu ya Syria.
Katibu Mkuu pia amewasihi wasyria ambao wamekubali mwaliko wa majadiliano, kujihusisha kwa nia njema baada ya miaka sita ya kumwaga damu akisema kuwa anatambua mchakato huo hautakuwa rahisi, lakini akasema njia pekee ya amani ya Syria ni suluhu ya kisiasa.