Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watoto milioni 1.4 wako katika hatari ya kifo sababu ya baa la njaa - UNICEF

Takriban watoto milioni 1.4 wako katika hatari ya kifo sababu ya baa la njaa - UNICEF

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema takriban watoto milioni 1.4 wako katika hatari ya kifo kutokana na utapiamlo mkali mwaka huu kwa sababu ya baa la njaa nchini Nigeria, Somalia, Sudan Kusini na Yemen .

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake amesema  muda unayoyoma kwa watoto zaidi ya milioni moja lakini ameongeza kuwa bado kunauwezekano wa kuokoa maisha ya wengi. Bwana Lake amesema utapiamlo na njaa ni changamoto zinazosababishwa na mwanadamu na zinaweza kutatuliwa kwa kasi, akionya kutorejea tena zahma ya 2011 ya baa la njaa katika pembe ya Afrika.

Taarifa ya UNICEF inasema kaskazini mashariki mwa Nigeria, idadi ya watoto wenye unyafuzi inatarajiwa kufikia 450,000 mwaka huu katika majimbo yenye misukosuko ya vita ya Adamawa, Borno na Yobi.

Nako Somalia, hali ya ukame ni tishio kubwa kwa idadi ya watu ambao tayari wameshuhudia vita kwa miongo kadhaa. Karibu nusu ya idadi ya watu, au watu milioni 6.2 nchini humo wanakabiliwa na ukosefu wa uhakika wa chakula na wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Nchini Sudan Kusini, nchi iliyokumbwa na mgogoro, umaskini na hali ya usalama ikiwa  tete,  zaidi ya watoto 270,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkubwa. Njaa ikiwa imetangazwa katika maeneo ya Jimbo la Unity kaskazini na katikati mwa nchi, ambapo kuna watoto 20,000. Jumla ya idadi watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula inatarajiwa kuongezeka kutoka milioni 4.9 hadi milioni 5.5.

Yemen nayo  ikiwa imekabiliwa na mgogoro kwa miaka miwili iliyopita,  zaidi ya watoto 462,000 wanasumbuliwa na utapiamlo mkali – hii ni ongezeko la karibu asilimia 200 tangu 2014.

Mwaka huu UNICEF inafanya kazi na washirika ili kutoa matibabu kwa watoto 220,000 wanaokabiliwa na utapiamlo nchini Nigeria, 200,000 Sudan Kusini, zaidi ya  watoto 200,000 wengine nchini Somalia na watoto 320,000 nchini Yemen.

Photo Credit
Picha: UNICEF