Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Sudan Kusini huko Ethiopia kupata makazi- IOM

Wakimbizi wa Sudan Kusini huko Ethiopia kupata makazi- IOM

Pakua

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM baadaye mwezi huu litajenga makazi ya muda kwa wakimbizi wa Sudan Kusini walioko jimbo la Gambella nchini Ethiopia.

Mkuu wa ofisi ndogo ya IOM huko Gambella, Miriam Mutalu amesema makazi hayo yapatayo 900 yatajengwa kwenye kambi mpya ya Nguennyiel ambayo ilifunguliwa mwezi Septemba mwaka jana kwa ajili ya wakimbizi 4,400.

Kwa sasa kambi hiyo inahifadhi wakimbizi 27,620 kutoka Sudan Kusini, idadi ambayo inaonekana inaweza kuongezeka kwa kuwa hakuna dalili ya mzozo nchini mwao kumalizika.

Bi. Mutalu amesema ujenzi wa makazi hayo ya muda unaotokana na usaidizi wa Uingereza, unaashiria kuboreshwa kwa makazi ya sasa ya dharura yaliyoezekwa kwa makaratasi ya nailoni na ambayo hufanya mazingira kuwa magumu msimu wa joto kali.

Photo Credit
Wakimbizi kutoka Sudan Kusini walioko katika eneo la Gambella nchini Ethiopia wakihamishwa.(Picha:IOM)