Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zahma na vita vyahatarisha uhakika wa chakula

Zahma na vita vyahatarisha uhakika wa chakula

Pakua

Shirika la Chakula na Kilimo, FAO limesema nchi 39 ulimwenguni zinategemea msaada wa chakula kutokana na vita na majanga ya asili.

FAO imesema hayo katika ripoti yake iliyotolewa Alhamisi iitwayo "Matarajio ya mazao na hali ya chakula", ikitaja Cameroon na Chad kuwa miongoni mwao na hilo limesababishwa na kulemewa na idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi jirani.

Halikadhalika imetaja Sudan Kusini ambapo migogoro mikubwa imekwamisha shughuli za kilimo wakati nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati mapigano yameleta hasara na upungufu wa rasilimali katika kaya.

Imeongeza kuwa mgogoro unaoendelea katika majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria na kushuka kwa sarafu ya naira kumechangia watu milioni 8 nchini hu mo kuhitaji msaada wa chakula na idadi hiyo inatarajiwa kupanda na kufikia milioni 11 ifikapo 2017.

Ripoti imesema idadi kubwa ya watoto waliodumaa kutokana na umasikini uliokithiri imeathiri Madagascar, Malawi na Msumbiji, ambako uzalishaji wake umeathiriwa na dhoruba ya El Nino.

 Nchi zingine zilizotajwa ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Eritrea, Kenya, Lesotho, Liberia, Libya, Madagascar, Malawi, Mali, Sierra Leone, Somalia, Uganda na Zimbabwe.

Photo Credit
Picha: UNICEF/UN028762/Tremeau