Skip to main content

Watoto Mosul watibiwa majeraha ya risasi- WHO

Watoto Mosul watibiwa majeraha ya risasi- WHO

Pakua

Shirika la afya duniani, WHO linasema mapigano yakiendelea huko Mosul nchini Iraq watoto wenye umri hata wa miezi miwili wamebainika kuwa na majeraha ya risasi na sasa wanapatiwa matibabu.

WHO inasema watoto hao ni miongozni mwa raia 1,200 wakiwemo wanawake, watoto na watoto wachanga ambao wamekabiliwa na majeraha tangu vikosi vya Iraq vianze mashambulizi dhidi ya magaidi wa ISIL kwenye mji huo wiki tano zilizopita.

Ingawa waliojeruhiwa wameshatoka upande wa Mashariki mwa Mosul, WHO inasema bado raia wengi wenye majeraha wamenasa mjini humo.

Fadela Chaib ni msemaji wa WHO, Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Fadela)

“Maeneo yanayozunguka Mosul yaliyokumbwa na mapigano hayana idadi kubwa ya watu hivyo idadi ya watu waliokumbwa na kiwewe ni ndogo. Mapigano yanavyoendelea mjini humo tunatarajia idadi kubwa zaidi ya majeruhi miongoni mwa raia kwa sababu hatuna taarifa za kina kuhusu hali ya hospitali mjini Mosul.”

Pamoja na kliniki zinazotoa huduma kutoka eneo hadi eneo, WHO imeweka vituo vya dharura vya kusaidia majeruhi kwenye eneo lililo kilometa 25 kutoka Mosul, ambako wagonjwa waliokumbwa na kiwewe na majeruhi mengine wanaweza kupata huduma ya kuokoa maisha yao.

Photo Credit
Watoto ni waathrika wa mzozo Mosul.(Picha:S. Baldwin/UNHCR)