Twataka mshikamano thabiti kwa wasichana wa Chibok- Wataalamu
Watalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa serikali ya Nigeria na wanachi wake kuwapatia mshikamano thabiti wasichana 21 waliochiliwa huru na kundi la Boko Haram.
Katika taarifa yao ya pamoja wataalamu hao wamesema pamoja na kupongeza mamlaka za Nigeria kwa kufanikisha kuachiliwa huru wasichana hao, serikali sasa iwafuatilie ili wapatiwe huduma za msingi haraka iwezekanavyo ikiwemo ulinzi.
Wataalamu hao Maud de Boer-Buquicchio kuhusu watoto, Urmila Bhoola kuhusu utumwa na Dainius Pûras anayehusika na haki ya afya wamesema usaidizi huo utawaepusha wasichana hao na vikwazo kama vile kunyanyapaliwa, kutengwa, kunyimwa huduma za afya na vitisho.
Wamesema kuwapatia msaada wa kujumuika na jamii siyo tu wajibu kwa kimaadili bali pia wa kisheria kwa mujibu wa vipengele vya sheria za kimataifa.