Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaongeza operesheni za dharura Kusini mwa Madagascar

WFP yaongeza operesheni za dharura Kusini mwa Madagascar

Pakua

Ukame ulioendelea kwa mwaka wa tatu mfululizo, umeongeza madhila kwa maelfu ya watu Kusini mwa Madagascar, na shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) linaongeza operesheni zake za kibinadamu ili kukabiliana na ongezeko la njaa na utapiamlo.

Matokeo ya awali ya tathimini ya mashirika mbalimbali kuhusu uhakika wa chakula, yatatolewa hivi karibuni, na yanaonyesha kwamba wilaya nne kati ya tisa za Kusini mwa Madagascar zinauwezekano wa kuwa katika hali ya dharura huku wilaya nyingine tatu zitafuata nyayo kusipochukuliwa hatua madhubuti ifikapo mwisho wa mwaka.

Mkurugenzi mkuu wa WFP Ertharin Cousin baada ya kuhitimisha ziara yake kisiwani humo amesema hali inatia hofu. Njaa na utapiamlo walioushuhudia ni matokeo ya mavuno hafifu kwa miaka mitatu mfululizo.

Amesema ni lazima fedha za ufadhili zipatikane sasa kabla ya kuchelewa na hali kuwa mbaya zaidi. Fedha hizo pia zitaruhusu kuwekeza katika maisha ya watu, ili isiwe tuu kuokoa maisha bali pia kubadili maisha na kuvunja mzunguko wa huduma za dharura.

Kusini mwa Madagascar kumeathirika pakubwa na El Niño, iliyosababisha mvua kuwa haba eneo zima la Kusini mwa Afrika.

Photo Credit
Nchini Madagascar. Picha ya FAO.