Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 17 wauawa katika ghasia huko DRC

Watu 17 wauawa katika ghasia huko DRC

Pakua

Huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, kumetokea mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama ambapo watu 17 wamefariki dunia, miongoni mwao raia 14 na polisi watatu.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa mapigano hayo yametokea majira ya leo asubuhi kabla ya maandamano ya kutaka Rais Joseph Kabila ajiuzulu, maandamano ambayo yalifutwa na serikali.

Kufuatia ripoti hizo za vifo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameelezea wasiwasi wake juu ya ghasia hizo Kinshasa na kwenye maeneo mengine ya DR Congo akilaani ghasia zilizotokea.

Ban ametoa wito kwa viongozi wote wa kisiasa na wafuasi wao kujizuia na ghasia zinazoweza kusababisha hali kuwa mbaya zaidi.

Ametaka mamlaka za DR Congo kuhakikisha kuwa vikosi vya usalama vinajizuia kutumia nguvu kupita kiasi wakati wanapochukua hatua dhidi ya maandamano.

Halikadhalika amesihi viongozi wa kisiasa kumaliza tofauti zao kwa njia ya mashauriano kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2277 la mwaka 2016.

Photo Credit
UN Photo/Rick Bajornas)