UM walaani uvamizi kwenye hospitali Kaga Bandoro huko CAR

UM walaani uvamizi kwenye hospitali Kaga Bandoro huko CAR

Pakua

Mratibu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Dkt. Michel Yao amelaani uvamizi uliofanywa na watu wenye silaha kwenye hospitali moja huko Kaga Bandoro kaskazini mwa nchi hiyo.

Dkt. Yao ambaye pia ni mwakilishi mkazi wa shirika la afya ulimwenguni nchini CAR ametoa wito badala yake maeneo kama hayo yaheshimiwe ikiwemo majengo ya afya na wafanya kazi wake.

Yaelezwa kuwa mnamo tarehe 12 mwezi huu, watu wenye silaha waliingia katika hospitali hiyo wakidai huduma kwa mmoja wao aliyejeruhiwa na kuwashurutisha wafanyakazi wa huduma hizo na wagonjwa wengine.

Mratibu huyo ameonya juu ya unyanyasaji dhidi ya wafanyakazi wa afya, ukiukaji wa sheria za kimataifa na kusema kuwa vikundi mbali mbali vya waasi na jeshi lazima viheshimu maeneo ya kutoa huduma na wafanya kazi wa afya.

Halikadhalika amewakumbusha wafanyakazi wote wa afya upande wowote, kutokuwa na upendeleo na kuimarisha amani na kuleta mshikamano wa jamii.

Photo Credit
Watu waliofurushwa makwao na kukimbilia uwanja wa kanisa.(Picha:UNHCR/B. Heger)