Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfahamu Patrice Lumumba kupitia simulizi ya Brian Urquhart wa UM

Mfahamu Patrice Lumumba kupitia simulizi ya Brian Urquhart wa UM

Pakua

Patrice Lumumba, Waziri Mkuu wa kwanza wa taifa huru la Congo, alihudumu kwa wiki kumi tu madarakani, lakini amesalia kuwa mtu mashuhuri na shujaa- kwa baadhi ya watu na kwa wengine jitu la kutisha! Enzi za ukoloni wa Ubelgiji, Lumumba alikuwa karani wa posta na baadaye mchuuzi wa bia. Akiwa kiongozi wa chama cha Mouvement Nationale Congolais (MNC) alikamatwa na wakoloni kwa sababu ya maandamano na kuswekwa rumande huko Stanleyville mwaka 1959 na baadaye aliachiwa huru ili ashiriki kwenye mazungumzo ya uhuru wa Congo.

Uhuru ukinukia aliteuliwa Waziri Mkuu.Umaarufu wake uliibuka wakati wa sherehe za uhuru wa Congo tarehe 30 Juni 1960 baada ya mfalme Baudoin wa Ubelgiji kutumia fursa ya sherehe hizo kutetea  yale yaliyofanywa na Ubelgiji nchini humo.Joseph Kasa-Vubu, Rais wa kwanza wa Congo wakati huo  alijibu hotuba hiyo kwa heshima na taadhima lakini Lumumba alipochukua kipaza sauti hakusitiri neno. Akatumbua jipu na kukemea ukoloni wa wabelgiji akisema ulikuwa ni dhihaka kubwa. Ubelgiji haikutarajia kwani ilitegemea baada ya uhuru mambo yataendelea kama ada.Siku tano baada ya uhuru askari wa jeshi la Congo ambalo hakukuwepo na afisa hata mmoja wa kicongo, wakakengeuka na kuanza kushambulia raia wa kibelgiji. Ubelgiji ilishindwa kuchukua hatua huku harakati za kugombea miji mbali mbali zikiendelea.

Ndipo Ubelgiji ikajikita jimboni Katanga kwenye utajiri mkubwa, jimbo ambalo lilijitenga. Rais Kasa-vubu na Waziri Mkuu wakeLumumba walisaka usaidizi kutoka Marekani kwa Rais Eisenhower bila mafanikio yoyote na hivyo wakabisha hodi Umoja wa Mataifa. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likaidhinisha kupelekwa kwa kikosi kikubwa cha walinda amani ili kuoondoa askari wa kibelgiji huko Congo na kurejesha utulivu wa raia na utawala. Kikosi cha kwanza cha askari 3,000 kutoka nchi za Afrika kiliwasili ndani ya siku tatu,  na wengine 10,000 waliwasili wiki mbili baadaye kukiwa na watendaji ili kuondoa pengo la utawala wa raia, huduma za afya, mawasiliano na usalama. Nia ikiwa kuelekeza wanaCongo jinsi ya kuongoza nchi  yao.

image
Tarehe 24 Julai mwaka 1960, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Congo, Patrice Lumumba alipotua uwanja wa ndege New York, Marekani kwa ajili ya ziara yake Umoja wa Mataifa. (Picha:UN/Maktaba)
Katanga ilijitenga, wanajeshi wa kibelgiji wakiendelea kuwepo huku vikosi vya Umoja wa Mataifa vikiwa havina mamlaka ya kuwashambulia bali kuweka majadiliano. Lumumba hakufurahi Alisaka usahiba na Urusi huku vyombo vya habari vya magharibi vikidai ni kibaraka wa nchi hiyo, jambo ambalo baadaye lilimchochea kusaka usaidizi wa kijeshi kutoka Urusi ambapo ndege 11 za mizigo ziliwasili Stanleyville zikiwa na bendera ya Congo na zimeandikwa Jamhuri ya Congo.

Lumumba hata alitishia kufukuza kikosi cha Umoja wa Mataifa na yaelezwa kuwa mapema mwezi Septemba baada kuomba usaidizi wa kijeshi kutoka Urusi, shirika la ujasusi la kimarekani, CIA lilipatiwa kibali kumuua, lakini walishindwa wakati huu kutokana na ulinzi mkali kutoka Umoja wa Mataifa. Lumumba alisaka kumaliza harakati za kujitenga kwa jimbo la Kasai. Alibeba askari kwa kutumia ndege za kisovieti kwenda Katanga ambapo askari walijitwalia madaraka na hata kuripotiwa vitendo vya ubakaji na uporaji kwa watu wa jamii ya Luba.

Hii ilimjengea uadui mkubwa. Kitendo hiki kilimchochea Rais Kasa-Vubu na kwa ushawishi wa Marekani, alimuondoa Lumumba serikalini kwa madai ya kutumbukiza taifa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Lumumba alijibu hoja kupitia redioni na kutoa wito kwa wananchi wa Congo kusimama kidete na kupambana ili wafe nae. Kwa kuwa nchi za magharibi zilimuunga mkono Rais Kasa-Vubu huku Urusi ikimuunga mkono Lumumba , Congo iligawanyika pande mbili, Mashariki na Magharibi huku Umoja wa Mataifa ukiwa kati. Siku chache baadaye mambo yalibadilika baada ya mnadhimu mkuu wa Lumumba,

Kanali Joseph Mobutu alipohamia upande wa pili.  Kufuatia ushawishi wa Marekani, Mobutu alitangaza kupitia radio kuwa anachukua serikali akiwa mrengo wa Rais Kasa-Vubu na kuwa kiongozi mkuu wa serikali. Lumumba, akiwa chini  ya ulinzi wa vikosi vya Umoja wa Mataifa aliendelea kuishi akiwa ametengwa kwenye makazi ya Waziri Mkuu lakini zama zake za utawala zimefika ukingoni. Pindi Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipolazimika chini ya shinikizo la Marekani kupiga kura kumtambua Kasa-Vubu na Mobutu kuwa wakaliaji halali wa kiti cha Congo kwenye Baraza Kuu la Umoja huo, ndipo Lumumba alitambua kama karata kishalamba garasa mchezo umekwisha.

image
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Congo, ambayo baadaye ilijulikana kama Zaire na sasa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo akiwa katika mazungumzo na mmoja wa watu wa ujumbe wake kabla ya kuzungumza na wanahabari kwenye makao makuu ya UM, New York, Marekani. (Picha:UN/Maktaba)
Tarehe 25 novemba mwaka 1960 akiwa amejificha kwenye kiti cha nyuma cha gari huku mvua kubwa ikinyesha aliondoka kisiri kwenye makazi yake ili kusaka kuungwa mkono huko kwenye ngome yake Stanleyville. Jeshi la Umoja wa Mataifa halikuruhusiwa kujihusisha na siasa za Congo na hivyo liliagizwa lisijihusishe na harakati za Lumumba wala wafuasi wake. Alikamatwa na askari wa Mobutu na kutiwa korokoroni huko Thysville.

Hata akiwa gerezani, Lumumba alikuwa tishio kwa Kasa-Vubu,  Mobutu, lakini pia kwa Marekani na Ubelgiji. Kwa hiyo wakati Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Dag Hammarskjöld na wawakilishi wake wakipigania aachiliwe huru, Kasa-Vubu na Mobutu, kwa usaidizi wa Ubelgiji walikuwa wanasaka mbinu za kummaliza kabisa.

Hivyo mpango ulisukwa kumkabidhi Lumumba kwa watu wa Kasai waliotaka kulipiza kisasi. Ndege ilimchukua Lumumba na wenzake watatu, ndani ya ndege walipata kipigo na mateso makali na baada ya kutua Katanga walipelekwa eneo la mafichoni ambako waliuawa na kuzikwa. Siku iliyofuatia miili  yao ilifukuliwa, ilikatwakatwa na kuyeyushwa kwenye tindikali ya Sulfa. Mpaka leo hii mabaki ya miili yao iliko ni kitendawili kisicho na jibu , wakati huo Patrice Lumumba alikuwa yu ngali kinda mwenye umri wa miaka 36 tu.

Photo Credit
24 Julai 1960 – Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Congo, sasa DRC, Patrice Lumumba, alipotembelea makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. (Picha:UN/MB