Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utumaji fedha kutoka ughaibuni moja ya mbinu mpya ya kufadhili maendeleo -UNCTAD

Utumaji fedha kutoka ughaibuni moja ya mbinu mpya ya kufadhili maendeleo -UNCTAD

Pakua

Nchi za Afrika zinapaswa kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato ili kufadhili maendeleo yao, la sivyo utegemezi wa mikopo utakwamisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya kuhusu maendeleo ya kiuchumi barani Afrika iliyozinduliwa leo Nairobi, Kenya na kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD.

Akizindua ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi ametaja vyanzo hivyo ni pamoja na pesa zinazotumwa na waafrika walio ughaibuni, udai kati ya sekta binafsi na umma na kuhakikisha zinadhibiti usafirishaji haramu wa fedha.

Mwandishi wa ripoti hiyo, Junior Roy Davis ameieleza Radio ya Umoja wa Mataifa kile kinapaswa kufanyika ili utumaji wa fedha usisalie karaha kwa wale wanaotuma.

(Sauti ya Junior)

"Nchi hazitumii vizuri fursa hii ya utumaji fedha kama ambavyo wangaliweza. Moja ya njia tunazopendekeza hili linaweza kushughulikiwa iwapo benki zao barani Afrika zitatoa kiwango cha kubadilisha fedha kwa kuzingatia akaunti za fedha za kigenijambo ambalo litahamasisha walio  ughaibuni kutuma fedha kwa usalama bila kukumbwa na hasara itokanayo na kubadilisha fedha kwa viwango tofauti."

Junior amesema Kenya iko mbele zaidi katika kurahisisha wale walioko ughaibuni kutuma fedha nyumbani na hivyo kujipatia kipato.

Amesema mipango mizuri ya kuwezesha walio ughaibuni kutuma fedha nyumbani inasaidia kwa kuwa..

(Sauti ya Junior)

"Ni nzuri kwa nchi kwani  ni mfumo rasmi wa mtiririko wa fedha . Inajenga uchumi wa benki za ndani, na hela hizo zaweza kuwekezwa na kusaidia kujenga uwezo wa kuzalisha katika nchi.''

UNCTAD inasema utumaji fedha kutoka ughaibuni kwa mwaka ni dola bilioni 63 za kimarekani, kiwango cha juu zaidi kuliko hata misaada ya kigeni.

Photo Credit
UN Photo/Sophia Paris