Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bomoabomoa Ukingo wa Magharibi yalaaniwa na UNRWA:

Bomoabomoa Ukingo wa Magharibi yalaaniwa na UNRWA:

Pakua

Kiwango kikubwa cha bomoabomoa kwenye jamii ya wakimbizi wa kibedui kwenye eneo la Anata linalokaliwa kwenye Ukingo wa magharibi, imelaaniwa vikali na shirika la Umoja wa mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.

Majengo saba ya makazi ya watu, malazi manne ya wanyama na vyoo vine vya umma vimebomolewa kwa mujibu wa msemaji wa UNRWA Chris Gunness. Matokeo yake amesema, familia saba zilizoorodheshwa na UNRWA zikiwa na jumla ya watu 43 , wakiwemo watoto 25 zimetawanywa na kubaki bila makazi.

Bwana Gunness ametoa wito kwa Israel kama taifa linalokalia makazi ya wengine kutekeleza mkataba wa nne wa Geneva ambao unataka kuheshimu haki za familia ikiwemo majengo ya watu wanaolindwa. Bwana Gunness ameelezea Israel kutofuata sheria za kimataifa kama ni hatua ya kushangaza na kuhuzunisha.

Timu ya UNRWA hivi sasa inatoa msaada kwa wakimbizi walioathirika na bomoabomoa hiyo pamoja na familia zao.

Photo Credit
Nembo ya UNRWA:Picha na UM/UNRWA