Skip to main content

Mkwamo wa mwelekeo wa uchaguzi DRC watia hofu- UM

Mkwamo wa mwelekeo wa uchaguzi DRC watia hofu- UM

Pakua

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu hali ya amani na  usalama huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, ambapo wajumbe wameelezwa kuhusu mvutano wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Jan Eliasson ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, aliwasomea wajumbe ripoti ya Katibu Mkuu ambayo inaeleza bayana mkwamo kuhusu kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.

Ripoti inataja mvutano kati ya serikali na wapinzani ambapo Rais Joseph Kabila alitangaza mwezi uliopita umuhimu wa kufanyika mjadala wa kisiasa kuhusu mustakhbali wa uchaguzi.

Hata hivyo hakuna makubaliano juu ya jinsi ya kufanyika mjadala huo na nani atashiriki huku wapinzani wakidai kuwa hiyo ni mbinu ya Rais Kabila ya kujiongezea muda wa uongozi baada ya Novemba 2016.

Hivyo Bwana Eliasson amesema..

(Sauti ya Eliasson)

“Mjadala shirikishi na halali baina ya wadau wa DRC ndio njia halali na pekee ya kuondoa mvutano wa kisiasa, kukabili mkwamo wa uchaguzi na kuzuia ghasia.”

Kwa upande wake, mwakilishi wa kudumu wa DRC kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Ignace Gata Mavita amesema..

(Sauti ya Balozi Mavita)

 “Kila mara, kama ambavyo tumewahi kusema, mjadala wa kitaifa wa kisiasa ambao tutajumuisha watu wote, ni muhimu liwe jambo la wakongo wenyewe ambapo watazungumza baina yao kama ambavyo inafanyika kwingineko.”

Photo Credit
UN Photo/Amanda Voisard (MAKTABA)