Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa hatua za mageuzi kuhusu ubinadamu- Ban

Ni wakati wa hatua za mageuzi kuhusu ubinadamu- Ban

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema sasa ndio wakati wa kuchukua hatua madhubuti kwa minajili ya kushughulikia mahitaji makubwa ya kibinadamu, na kwamba dunia sasa hivi inakabiliwa na changamoto ya aina yake.

Ban amesema hayo katika taarifa iliyochapishwa leo kwenye tahariri ya gazeti la The Guardian, ambapo ameandika kuwa watu milioni 130 kote duniani wanahitaji usaidizi wa kibinadamu, wakati watu zaidi ya milioni 60 wakiwa wamelazimika kuhama makwao.

Katibu Mkuu amesema, licha ya kwamba watu hao wanaishi katika mazingira magumu, kuna uhaba mkubwa wa ufadhili wa kuwasaidia, na hivyo kuibua maswali kuhusu mshikamano wa kimataifa katika dunia yenye utajiri mkubwa.

Akizungumza kuhusu mkutano wa dunia kuhusu masuala ya kibinadamu (WHS) uliomalizika nchini Uturuki mwezi Mei, Ban amesema mkutano huo haukuwa kituo cha ukomo, bali kituo cha kugeuza mwelekeo, na kwamba kuna haja ya kuzigeuza ahadi zilizotolewa katika mkutano huo kuwa vitendo.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unadhamiria kuimarisha juhudi zake kutokana na kasi ya mkutano huo, kwa kushirikiana na viongozi wa dunia na wadau wengine, kwa minajili ya kuwasaidia walio wadhaifu zaidi duniani.

Photo Credit
Katibu Mkuu Ban Ki-moon (picha ya UM)