Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malcorra ataka ustawi wa pamoja wa binadamu na dunia

Malcorra ataka ustawi wa pamoja wa binadamu na dunia

Pakua

Mgombea wa 11 wa nafasi ya ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Susana Malcorra, leo mchana amejieleza mbele ya wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja huo pamoja na vikundi vya kiraia,  ikiwa ni utaratibu wa aina yake ambao Baraza hilo limejiwekea katika kupata mrithi wa Ban Ki-moon anayehitimisha jukumu lake mwishoni mwa mwaka huu.

Katika hotuba yake, Bi. Malcorra ambaye ni Waziri wa mambo ya nje na masuala ya kuabudu wa Argentina amesisitiza mambo kadhaa ikiwemo umuhimu wa Umoja wa Mataifa kupitia sekretarieti na mashirika yake kufanya kazi kwa lengo la ustawi wa binadamu wote na sayari ya dunia.

Amesema katika dunia ya leo, ili kufanikiwa ni lazima kusikiliza watu kwa umakini na kufanya kazi kwa pamoja na wadau katika ngazi ya taifa, kikanda na kimataifa.

Hata hivyo amesema ili kufanya kazi kwa tija…

 

(Sauti ya Malcorra)

 

“Umoja wa Mataifa kusubiri matokeo ndio uchukue hatua hakuna tija yoyote. Umoja wa mataifa unapaswa kuwa na mpango wa kutarajia na kuzuia majanga duniani. Mtizamo wetu wa ustawi wa pamoja kati ya binadamu na dunia vinapaswa kuwa katika misingi yetu ya kusongesha maendeleo endelevu kama ilivyo kwenye ajenda 2030 na kupunguza matatizo ya muda mrefu. Kujenga uhimili  kunahitaji kujumuisha wanawake na vijana kama sehemu ya suluhu ya matatizo.”

Halikadhalika amesema Katibu Mkuu anatakiwa ajenge utamaduni wa unyenyekevu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya chombo hicho, sanjari na kutekeleza kwa nia njema maamuzi ya nchi wanachama na michakato yao ya kupitisha maamuzi hayo.

Photo Credit
Susana Malcorra. (Picha:UN/Manuel Elias)