Ushiriki wa NGOs ndani ya Umoja wa Mataifa wahitajika

Ushiriki wa NGOs ndani ya Umoja wa Mataifa wahitajika

Pakua

Mashirika yasiyo ya kiserikali yatawezeshwa na Umoja wa Mataifa ili kuongeza uwezo wao wa kushawishi na kushinikiza serikali katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu.

Hayo yameafikiwa kwenye mpango kazi wa kimataifa uliopitishwa leo mjini Gyeongju, nchini Jamhuri ya Korea, ikiwa ni siku ya mwisho ya kongamano la kila mwaka la idara ya mawasiliano ya Umoja wa Mataifa DPI na mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs.

Akizungumza kwenye hafla ya kufunga kongamano hilo, mkuu wa DPI Christina Gallach amesema mkutano huo umekuwa fursa ya kuonyesha umuhimu wa kujenga ubia zaidi kati ya Umoja wa Mataifa, vyuo vikuu na NGOs.

Aidha kwa mara ya kwanza wawakilishi wa vijana wamepitisha azimio likisisitiza umuhimu wa kushirikisha vijana zaidi kwenye uongozi na mchakato wa kuchukua uamuzi, pamoja na kuelimisha kizazi kipya kuhusu maadili ya uraia wa kimataifa.

Akizungumza na redio ya Umoja wa Mataifa, mwakilishi wa wanawake wa jamii asilia za Peul nchini Chad, Hindou Oumarou Ibrahim ameeleza atakachofanya baada ya mkutano huo.

(Sauti ya Hindou)

" Tutakachofanya na hati iliyotolewa, ni kuitafsiri kwenye lugha ambayo watu wanaweza kuielewa, na kuona jinsi ya kushirikisha watu wote ili kufuatilia matokeo ya kazi hiyo. Tunajua ni muhimu sana, kwa sababu mapendekezo mengi hayatekelezwi. Cha msingi ni ushiriki wa raia, ambao unaanza na kusoma hati na kuangalia jinsi ya kuitekeleza." 

Photo Credit
Vijiana wa Jamhuri ya Korea wakishiriki kongamano la DPI/NGO. Picha ya UN/Mjumbe maalum wa Vijana.