Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

#WHS: Twahitaji kipaumbele kwa wakimbizi na wahamiaji- AbuZayd

#WHS: Twahitaji kipaumbele kwa wakimbizi na wahamiaji- AbuZayd

Pakua

Kuelekea mkutano wa utu wa kibinadamu, #WHS, unaoanza kesho huko Istanbul, Uturuki, mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu wimbi kubwa la misafara ya wakimbizi na wahamiaji, Karen AbuZayd ametaka jamii ya kimataifa kupatia kipaumbele wahamiaji na wakimbizi.

Akihojiwa na kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa huko Istanbul, Bi AbuZayd amesema kipaumbele ni muhimu kwa kuwa idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanakimbia taabu na mateso huku kule wanakokimbilia nako uwezo unatindikia hivyo akasema matarajio ya mkutano ni...

(Sauti ya Karen)

“Nadhani itasaidia sana iwapo mkutano huu utaibuka na kiasi kikubwa cha utetezi kuhusu suala hili ili watu wapate uelewa zaidi. Kwa sababu kutakuwepo na majadiliano na kujifunza vitu vipya, Twatarajia watu wengi zaidi kuzungumzia suala hili na kushinikiza serikali zao kuchukua uamuzi sahihi mwezi Septemba.”

Amepigia chepuo nchi zilizofungua milango kwa wakimbizi na wahamiaji ikiwemo Canada akisema..

(Sauti ya Karen)

“Tuna mfano mzuri kabisa wa Canada ambayo ina mpango wa kufadhili familia, na inatueleza kuwa kuna familia zaidi ambazo zinataka kuchukua wakimbizi. Hii ni kwa sababu pindi unapokutana na mkimbizi au mhamiaji unabaini kuwa ni mtu kama mimi na ana haki ya kupata fursa kama nilizo nazo.”

Mkutano wa masuala ya utu wa kibinadamu unafanyika kwa siku nne huku Umoja wa Mataifa ukiangazia pia tarehe 19 mwezi Septemba mwaka huu ambapo kutafanyika kikao cha ngazi ya juu kuhusu wahamiaji na wakimbizi jijini New York, Marekani.

Photo Credit
Karen AbuZayd akihojiwa na Fabrice Robinet wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa. (Picha:UN/Stephanie Coutrix)