Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waomba sitisho la mapigano liimarishwe Syria

Umoja wa Mataifa waomba sitisho la mapigano liimarishwe Syria

Pakua

Sitisho la mapigano nchini Syria linatekelezwa kwa asilimia 50 tu, ikilinganishwa na asilimia 80 wiki chache zilizopita, amesema leo Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura, akiongeza kwamba bado mazungumzo ya amani baina ya pande za mzozo za Syria hayajafikia popote.

Amesema hayo akizungumza leo na waandishi wa habari mjini Vienna baada ya mkutano na mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na wa Urusi Serguei Lavrov.

Bwana De Mistura ameeleza kwamba kituo cha operesheni kilichopo mjini Geneva kwa ajili ya kufuatilia sitisho la mapigano kimeimarika kupitia ushirikiano wa kitaaluma wa Marekani na Urusi.

Kwa upande wa hali ya kibinadamu, Bwana de Mistura ameeleza kwamba misaada imeweza kufikia miji 12 tu kati ya 18 iliyozingirwa, huku usaidizi wa kibinadamu ukifikishwa kwa kuangushwa kutoka angani kwenye sehemu zingine.

Hatimaye Bwana de Mistura amesema changamoto nyingine anataka kukabiliana nayo ni hatma ya mamia ya watu waliofungwa au kukamatwa na serikali au vikundi vya waasi.

Photo Credit
UN Photo/Pierre Albouy