Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akiwa Nepal, Eliasson asema “Pamoja” ndilo neno muhimu zaidi duniani sasa

Akiwa Nepal, Eliasson asema “Pamoja” ndilo neno muhimu zaidi duniani sasa

Pakua

Neno “pamoja” ndilo neno muhimu zaidi katika dunia ya sasa, na hakuna mtu mmoja anayeweza kufanya kila kitu peke yake, lakini sote tunaweza kufanya kitu fulani.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, wakati wa ziara yake katika wilaya ya Sindhupalchowk nchini Nepal, ambayo ni moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na tetemeko la ardhi nchini humo, siku chache kabla ya mkutano kuhusu masuala ya kibinadamu mjini Istanbul, mwezi huu wa Mei, 2016.

Bwana Eliasson amewakumbusha waathirika wa tetemeko hilo la ardhi kwamba kila mtu ni sehemu ya familia ya Umoja wa Mataifa, na kwamba Umoja wa Mataifa utawasaidia katika jitihada za kujenga tena maisha yao.

Katika ziara hiyo, Bwana Eliasson amekutana na wanawake manusura na kutembelea pia kituo cha wanawake Irkhu. Mmoja wa wanawake aliokutana nao alipoteza familia yake yote, na kupewa makazi katika kituo hicho.

Aidha, Naibu huyo wa Katibu Mkuu amekutana na jamii ya wakulima katika kata iliyoathiriwa zaidi na tetemeko hilo la ardhi.

Photo Credit
Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson akiwa Nepal. (Picha: Pnud/Nepal)