Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada yazuiliwa Syria, mazungumzo yaendelea

Misaada yazuiliwa Syria, mazungumzo yaendelea

Pakua

Misafara ya misaada ya kibinadamu imeendelea kukumbwa na vikwazo kufikia wahitaji nchini Syria, amesema leo mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Mjumbe Maalum kwa Syria, Jan Egeland baada ya mkutano uliofanyika leo mjini Geneva Uswisi kuhusu ufikishaji misaada ya kibinadamu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Egeland ameeleza kwamba licha ya utaratibu mpya wa kuhakikisha utoaji kibali kwa misafara ya kibinadamu, misaada inazidi kuchelewa kufikia wahitaji serikali ikichelewa kutoa kibali hicho.

(Sauti ya bwana Egeland)

“Tulikuwa na misafara mitano iliyokuwa tayari kwenda kwa kipindi cha siku nne zilizopita, yote haikuweza kwenda. Kwa hiyo watu 287,000 hawakupata misaada kwenye maeneo yanayofikika kwa taabu au yaliyozingirwa.”

Hata hivyo amesema mashirika ya kibinadamu yanatarajia kuanzisha mradi wa kusafirisha kutoka maeneo hayo watu 500 walio hatarini kufa kwa sababu za kiafya.

Kwa upande wake Staffan de Mistura, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, amesema awamu nyingine ya mazungumzo ya amani inatarajia kuanza tarehe 13 mwezi huu mjini Geneva Uswisi. Hata hivyo amesema kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo atasafiri kwenda Urusi, Syria, Jordan, Lebanon na Iran ili kujadili na wadau mbalimbali na kukuza maelewano kuhusu mchakato huo wa amani.

Photo Credit
Msafara wa misaada ya kibinadamu ukielekea katika mji wa Madaya, Syria. Picha: OCHA Syria