Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laongeza muda wa mamlaka ya UNSOM

Baraza la Usalama laongeza muda wa mamlaka ya UNSOM

Pakua

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja limepitisha azimio namba 2275 (2016), la kuongeza muda wa mamlaka ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM, kwa kipindi cha mwaka mmoja, hadi Machi 31 mwaka 2017.

Likilaani vikali mashambulizi ya hivi karibuni ya kikundi cha Al-Shabaab na kukariri dhamira yake kuunga mkono juhudi za kupunguza tishio la kikundi hicho cha kigaidi, Baraza la Usalama limetilia msisitizo umuhimu wa UNSOM katika kusaidia mchakato wa kisiasa nchini Somalia, ikiwemo kuunga mkono harakati za amani na maridhiano, kukamilisha uundaji wa serikali na kufanyia marekebisho katiba, pamoja na kuandaa uchaguzi ulio jumuishi, huru, wa haki na wa wazi mwaka huu wa 2016.

Aidha, azimio hilo limekaribisha ushirikiano imara kati ya UNSOM na ujumbe wa Muungano wa Afrika, AMISOM, na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano huo hata zaidi.

Kupitia azimio hilo, Baraza la Usalama limemwomba Katibu Mkuu kufanyia tathmini uwepo wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia baada ya mchakato wa uchaguzi wa 2016, na kuhakikisha kuwa Umoja wa Mataifa umejiandaa ipasavyo kusaidia awamu itakayofuata ya ujenzi wa taifa la Somalia, na kutoa mapendekezo kwa Baraza hilo kufikia Januari 2017.

Photo Credit
Hapa ni walinda amani wa UNSOM wakati wa ziara la Baraza la Usalama nchini Somalia mwaka 2014.(Picha:UM/Tobin Jones)