Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani mashambulizi Brussels

UM walaani mashambulizi Brussels

Pakua

Umoja wa Mataifa umelaani vikali mashambulio ya kigaidi yaliyotokea leo huko Ubelgiji ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema mashambulio hayo yamegusa eneo ambalo ni kitovu cha Muungano wa Ulaya.

Mashambulio hayo mawili yametokea leo asubuhi kwenye uwanja wa ndege na kituo cha treni katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels ambapo watu wapatao 31 wameripotiwa kuuawa.

Ban ametuma rambirambi kwa wafiwa akiwatakia ahueni majeruhi akitaka wahusika wasakwe na wafikishwe mbele ya sheria.

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft amesema ameshtushwa na mashambulizi hayo akisema ni tukio hilo sambamba na yale ya karibuni humo Uturuki na Cote d’ Ivoire na yanapaswa kulaaniwa vikali.

Ameelezea mshikamano na wahanga akisema vitendo vya kigaidi haviwezi kuhalalishwa kwa misingi yoyote ile na kwamba katika zama za sasa ugaidi hauna nafasi na badala yake unaimarisha azma za serikali na dunia kwa ujumla kusaka mbinu za kufungulia mashtaka wahusika.

Kwa mantiki hiyo Bwana Lykketoft amesihi nchi zote kukabili ugaidi kwa njia zote zile huku zikizingatia wajibu wao kwa sheria za kimataifa na haki za binadamu na zile za wakimbizi.

Photo Credit
Rais wa baraza kuu la Umoja wa mataifa Mogens Lykettoft.(Picha:UM/Mark Garten)