UM waridhishwa na hukumu dhidi ya Jean-Pierre Bemba

UM waridhishwa na hukumu dhidi ya Jean-Pierre Bemba

Pakua

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein, amekaribisha hukumu iliyotolewa leo na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC kuhusu kesi ya Jean-Pierre Bemba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Haki za Binadamu imeeleza kwamba Bwana Bemba amekutwa na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita vikiwemo vitendo vya ubakaji, mauaji na uporaji ambavyo vilitekelezwa kati ya mwaka 2002 na 2003 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Bwana Zeid amesema kwamba anatumai hukumu hiyo itawazuia wengine kutekeleza ukiukwaji wa haki za binadamu, siyo tu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, bali pia popote unapotekelezwa.

Ameongeza kwamba anaamini hukumu hiyo ni hatua muhimu katika kupambana na ukatili wa kingono na ukwepaji sheria.

Jean-Pierre Bemba alikuwa Kamanda Mkuu wa kundi la waasi la MLC kutoka DRC ambalo liliingia Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2002 na 2003 kwa ajili ya kumsaidia rais Patassé kudhibiti jaribio la mapinduzi. Kundi hilo lilishtakiwa kutekeleza idadi kubwa ya vitendo vya uhalifu na ukatili wa kingono dhidi ya raia wa CAR.

Photo Credit
Jean-Pierre Bemba. Picha ya ICC/UNIFEED