Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Djinnit ataka dhima zaidi ya NGOs ukanda wa Maziwa Makuu

Djinnit ataka dhima zaidi ya NGOs ukanda wa Maziwa Makuu

Pakua

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa huko Maziwa Makuu Said Djinnit amesisitiza umuhimu ushirikishaji wa mashirika ya kiraia, NGOs kwenye juhudi za kukabili changamoto katika eneo hilo.

Amesema hayo jijini Dar es salaam, Tanzania kwenye jukwaa la mkutano wa kimataifa wa ukanda wa maziwa makuu, ICGLR ukileta washiriki wa mashirika ya kiraia kutoka ukanda huo.

Bwana Djinnit amesema mashirika hayo ni vyombo vinavyotambulika kisheria katika nchi zao na hivyo ni vyema yaondoe dhana potofu iliyoenea ya kutoaminika ili hatimaye kujenga udau thabiti na serikali.

Kauli hiyo ya Bwana Djinnit ilipigiwa chepuo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Augustine Mahiga aliyesihi mashirika hayo kujenga ushirikiano na serikali ili kuwa chachu ya mabadiliko.

Mkukano huo ulihudhuriwa na zaidi ya washiriki 60 kutoka nchi ambazo tayari zimechagua wawakilishi wa taasisi za kiraia ambazo ni DR Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia.

Nchi nne ambazo ni Angola, Burundi, Jamhuri ya Congo na Sudan bado kuchagua wawakilishi wao.

Photo Credit
Said Djinnit.(Picha:Ryan Brown)