Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la Geneva kuhusu Syria liwe fursa isiyopotezwa- de Mistura

Kongamano la Geneva kuhusu Syria liwe fursa isiyopotezwa- de Mistura

Pakua

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Stafan de Mistura, ametoa wito kwa watu wa Syria wapaze sauti ya pamoja kwa washiriki wa kongamano kuhusu Syria mwishoni mwa wiki hii, wakiwataka wasipoteze fursa inayotolewa na kongamano hilo.

Katika ujumbe aliourekodi kabla ya kuanza kongamano la pande kinzani za Syria jijini Geneva Uswisi, Bwana de Mistura amesema miaka mitano ya machafuko imekuwa muda mrefu sana, na kwamba kila mmoja anatambua bayana janga linalowakabili watu wa Syria.

Jueni kwamba tunawategemea kupaaza sauti yenu na kusema khalas, na itoshe! Mmwambie kila mtu anayekuja kutoka Syria na kutoka ng’ambo kwa kongamano hili, kwamba kuna matarajio kwao kuhakikisha kuwa maono yao, na uwezo wao kulegeza misimamo katika mazungumzo ili kufikia suluhu la amani Syria, ni sasa, na wanapaswa kuuonyesha sasa.”

Amesema mazungumzo katika kongamano hilo yanalenga kusongesha mbele hatua za kufikia utulivu na amani, na maisha ya utu nchini Syria, na kwamba kufuatia kufeli kwa makongamano mawili awali, hili halistahili kufeli

“Tumesikia sauti zenu, na tumesikia yale mmekuwa mkituambia mara nyingi tulipokutana nanyi, nyie watu wa Syria, nyie wanawake, wanume, na watoto wa Syria, mkisema: na itoshe, khalas, kefaya, na yakome mauaji, utesaji, jela. Na ukome uharibifu wa majengo”

De Mistura ameahidi uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa, akisema kwamba kamwe Umoja huo hautawatelekeza watu wa Syria.

Photo Credit
Staffan de Mistura, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mzozo wa Syria. (Picha:UN/Mark Garten)