Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti kuhusu usaidizi wa kibinadamu kuwasilishwa leo Dubai

Ripoti kuhusu usaidizi wa kibinadamu kuwasilishwa leo Dubai

Pakua

Jopo la ngazi ya juu kuhusu uchangishaji fedha kwa usaidizi wa kibinadamu hii leo linawasilisha ripoti yake ya mapendekezo ya jinsi ya kufanikisha harakati hizo kwenye mkutano unaofanyika leo huko Dubai, Falme za kiarabu.

Akizungumza na waandishi wa habari New York, Marekani, Kristalina Georgieva ambaye ni mwenyekiti mwenza wa jopo hilo amesema wameamua kuwasilisha ripoti hiyo mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon huko Mashariki ya kati kwa kuzingatia kuwa eneo hilo kwa sasa ni mfano dhahiri wa watu wenye uhitaji.

Ametolea mfano kuwa  maombi matatu ya fedha za usaidizi kati ya manne yanayozidi dola Bilioni Moja yanatoka ukanda huo.

Amesema kwa kuzingatia mahitaji yanayoongezeka kila uchao wameibuka na mapendekezo matatu ikiwemo, 

"Mosi kupunguza mahitaji ya usaidizi. Tunaamini kwa kuwekeza katika mfumo sahihi wa kuzuia majanga, utatuzi wa mizozo kutasaidia kupunguza mwelekeo huu ulioshika kasi sasa. Pili Tunahitaji kuongeza wigo wa upatikaji wa rasilimali.”

Ametaja pendekezo la tatu kuwa ni kwa wahisani na wadau kushirikiana na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inakuwa bora zaidi, mathalani misaada hiyo ipatikane kwa uhakika na iwe ya kutabirika.

Photo Credit
Mizozo inasababisha mahitaji kuongezeka kila uchao. Mathalani watoto hawa wakimbizi wa Palestina wakati wa msimu wa baridi nchini Syria. Picha ya UNRWA/Taghrid Mohammad