Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za simu za kiganjani zimeenea kuliko maji na umeme: Ripoti

Huduma za simu za kiganjani zimeenea kuliko maji na umeme: Ripoti

Pakua

Huduma za simu za kiganjani au rununu zimesambaa zaidi duniani hivi sasa kuliko umeme au maji.Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya Benki ya duniani kuhusu Intaneti ikitanabaisha kuwa hali hiyo inatokana na kupanuka kwa wigo wa teknolojia ya digitali.

Mchumi wa benki ya dunia Deepak Mishra amesema licha ya hali hiyo bado haimaanishi kuwa zama za mapinduzi ya digitali zimeibuka kwa kuwa bado hayajatimiza matarajio ya mapinduzi hayo kuleta manufaa kwa walio wengi ikiwemo serikali kuwajibika.

Mishra ambaye ni mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo amesema fursa ya mapinduzi hayo kuleta mabadiliko iko wazi lakini bado kuna changamoto kubwa kuliko vile ilivyotarajiwa.

Amesema mambo ya msingi ni serikali kuwa na sera thabiti kuhakikisha huduma inapanuka na inapatikana kwa urahisi kwa watu wote bila kujali walipo na pia ichochee ubunifu miongoni mwa jamii.

Ripoti inasema kuwa licha ya ongezeko la matumizi ya simu za mkononi, bado watu Bilioni Mbili duniani hawana huduma hiyo huku Nusu bilioni wakiishi maeneo yasiyo na mtandao wa simu hizo.

Photo Credit
Picha:WorldBank