Kenya iweke mustakhbali bora zaidi kwa wazee wote. Bi. Wamera
Malengo 17 ya maendeleo endelevu yanatarajiwa kupitishwa na wakuu na viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa baadaye mwezi huu kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani. Malengo hayo yanalenga kusongesha pale ambapo malengo ya maendeleo ya milenia, MDG yamekwamia.
Miongoni mwao ni lengo namba tatu ambalo linalenga afya na ustawi kwa watu wa umri wote bila kujali mtoto au mzee. Hata hivyo katika hali halisi baadhi ya nchi ni shubiri kwa wazee na wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Helpage International kuhusu hali ya wazee jijini New York, Marekani mmoja wa watoa mada alikuwa ni Bi. Esther Wamera kutoka Kenya ambaye katika mahojiano na Assumpta Massoi wa Idhaa hii alianza kwa kueleza mshtuko wake kuwa hata Kenya haikuwa miongoni mwa nchi 96 kati ya 194 zilizowasilisha takwimu kuhusu wazee. Je alipokea vipi?