Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

UNHCR yaonya kuongezeka machafuko ya magenge

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesikitishwa na kuongezeka kwa idadi ya watu wanokimbia machafuko ya megenge Amerika ya Kati, ambayo yanadaiwa kuwa makubwa ikilinganishwa na miaka 30 iliyopita.

UNHCR imesema inahofia idadi ya wanawake na watoto wasiosindikizwa ambao huishia kujumuishwa na makundi hayo, kukumbwa na mashambulizi ya kingono au mauaji.

Msemaji wa UNHCR Adrian Edwards amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa kuna kiwango cha juu cha machafuko katika nchi hizo kinachoongeza kiwango cha kusaka hifadhi.

Ulaya inakaribia kutokomeza surua na rubella:WHO

Nchi 32 barani Ulaya zimefanikiwa kudhibiti maambukizi ya maradhi ya surua na rubella kwa mujibu wa hitimisho la uhakiki wa kamisheni ya Ulaya ya kutokomeza surua na rubella uliotolewa leo.

Dr Zsuzsanna Jakab mkurugenzi wa kanda ya Ulaya wa shirika la afya duniani WHO amesema kudhibiti maambukizi ya maradhi hayo kwa zaidi ya nchi za Ulaya kunadhihirisha kwamba kutokomeza Surua na rubella katika kanda hiyo kunawezekana kwa kwamba wako katika njia sahihi ya kufikia lengo hilo.

Utapiamlo wapungua Rwanda, lakini kazi bado ipo

Utafiti mpya uliotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP na Wizara ya Kilimo ya Rwanda umeonyesha kwamba kiwango cha utapiamlo kimepungua kwa kiasi kikubwa nchini Rwanda kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, lakini bado kiko juu hasa kwenye maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa utafiti huo, uwiano wa watoto wenye umri wa chini wa miaka mitano waliodumaa umeshuka kutoka asilimia 43 mwaka 2013 hadi 36.7 mwaka 2015, tatizo hilo likikumba zaidi maeneo ya vjijini.

Hatma ya Ruto na Sang ICC kujulikana saa chache zijazo

Saa chache zijazo mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague Uholanzi itatoa uamuzi juu ya ombi la upande wa utetezi kwenye kesi dhidi ya William Ruto na Joshua arap Sang wote wa Kenya.

Upande wa utetezi uliomba kesi hiyo itupiliwe mbali kwa minajili kwamba hakuna kesi ya kujibu kwenye mashtaka dhidi ya wawili hao ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwemo mauaji, kuwafurusha watu makwao au kuwatoa watu makwao bila hiari yao na mateso.

Makosa hayo yadaiwa kufanyika mwaka wa 2007 na 2008 wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu.

Timu ya UM yaanza kukusanya taarifa za ubakaji CAR

Timu ya pamoja, ikiongozwa na Naibu Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Diane Cooper, imesafiri leo kwenda mkoa wa Kimo kwa mara ya pili, kama sehemu ya ujumbe wa kukusanya taarifa na kutafuta ukweli uliotangazwa wiki iliyopita.

Akitangaza hatua hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini New york, msemaji wa Katibu Mkuu Stephane Dujarric, amesema wajumbe hao pia wamekutana na wadau kadhaa mashinani.

Tuunge mkono kazi ya UNMAS- Mcheza filamu Daniel Craig

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu utokomezaji wa mabomu ya kutegwa ardhini na hatari ya vilipuzi, Daniel Craig, ametoa wito leo dunia iunge mkono kazi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloendesha shughuli za kuondoa mabomu ya kutegwa ardhini na jitihada za kibinadamu, UNMAS.

Bwana Craig amesema hayo mbele ya waandishi wa habari leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya kuelimisha kuhusu mabomu ya kutegwa ardhini na vifaa vya milipuko, leo tarehe 4 Aprili.

Uwepo wa mabomu ya ardhini bado ni tishio kubwa kwa maisha ya watu Afghanistan:UNAMA

Kuwepo kwa mabomu na vifaa vingine vya mlipuko nchini Afghanistan bado ni tishio kubwa kwa maisha na vipato vya maelfu ya raia wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti ya mpango wa Umoja wa mataifa nchini Afghanistan UNAMA, wakati wa mwaka 2015, Waafghanistan 388 waliuawa au kujeruhiwa kwa mabomu na vifaa vya mlipuko.

Aidha, vifaa vya milipuko vilikuwa hatari kubwa, na kusababisha majeruhi kwa raia 1,051 ikiwa ni pamoja na vifo 459 mwaka 2015.

Tusiwafeli watu wanaotuhitaji, wanapotuhitaji zaidi- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesisitiza umihimu mkubwa wa mashauriano na ushirikiano wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kufanikisha mkutano wa masuala ya kibinadamu, ambao utafanyika siku 50 tokea leo Aprili nne, jijini Istanbul, Uturuki.

Ban amesema, katika miaka mitatu iliyopita, ushiriki na michango ya nchi wanachama na wadau wengine, imesaidia kuendeleza mchakato wa mkutano huo wa kimataifa wa kiutu, ambao maandalizi yake yanaingia awamu ya mwisho, akigusia anachodhamiria kufanya,

WFP yazindua mpango wa mlo mashuleni kusaidia watoto wa Lebanon na Syria

Mwezi Machi shirika la mpango wa chakula duniani WFP limezindua mpango wa mlo mashuleni ambao unawasaidia watoto wa Lebanon na Syria 2wanaohudhuria shule za msingi za umma nchini Lebanon.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa wa WFP nchini Lebanon Dominik Heinrich elimu ni muhimu saana katika kuwawezesha vijana wa Lebanon na Syria kuwa na nyenzo ambzo wanahitaji ili kuchangia katika ukanda wao hasa katika wakati huu wa matatizo.