Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita ya Ukraine imetuletea adha dunia nzima: Azali Assoumani

Rais wa Comorrow Azali Assoumani akihutubia mjadala wa Baraza Kuu
UN Photo/Cia Pak
Rais wa Comorrow Azali Assoumani akihutubia mjadala wa Baraza Kuu

Vita ya Ukraine imetuletea adha dunia nzima: Azali Assoumani

Masuala ya UM

Rais wa kisiwa cha Comoro Azali Assoumani akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu kikao cha 77 amesema jumuiya ya kimataifa hivi sasa inakabiliwa na changamoto lukuki, kuanzia athari za kiafya kama janga la COVID-19 ambalo linaingia mwaka wa tatu ssasa, mabadiliko ya tabianchi hadi vita ya Ukraine ambayo imeleta adha kwa dunia nzima.

Rais Assoumani amesema mathalani janga la COVID-19 limeiathiri dunia nzima bila kujali nchi kubwa au ndogo, Tajiri au masikini na kudhihirisha kwanba hakuna mtu au taifa lililo na kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko na hivyo mshikamano wa kimataifa unahitajika katika kukabiliana na majanga kama hayo , kwa kupanga mikakatio ya kuzuia, kutibu, chanjo na ufadhili.

Amezipongeza juhudi zilizofanywa na wadau mbalimbali kukabiliana kwa haraka na janga hilo likiwemo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO.

Vita ya Ukraine 

Kuhusu vita ya Ukraine iliyotokana na uvamizi wa Urusi Rais huyo amesema imeleta adha kwa dunia nzima sio tu kwa kupandfisha bei ya mafuta na chakula bali kuongeza idadi ya wanaokabiliwa na njaa na kuathiri mfumo mzima wa maendeleo ikiwemo katika visiwa vya Comoro.

Ameongeza kuwa hali hiyo inahatarisha uhakika wa chakula duniani , uhaba wa chakula na baa la njaa kwani bei ya nafaka kama ngano mfani na ndio maana “Nchi yangu inalaani vikali uvamizi huo na tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuishawishi Urusi na Ukraine kuchukua njia ya mazungumzoa haraka iwezekanavyo na hiyo ndiyo njia pekee ya kumaliza uhasama unaoendelea.”

Ameendelea kusema mbali ya majanga ya afya, uhakika wa chakula na vita , jumuiya ya kimataifa inapaswa kuendelea kutatua changamoto za kisiasa , haki za binadamu na makundi ya walio wachache. 

Katika hilo ameendelea kuuomba Umoja wa Mataifa kusaka suluhu ya suala la waalestina na Israel kwa njia ya amani na kuhakikisha haki inatendeka kwa watu wa Palestina walioteseka kwa miaka mingi.

Masuala mengine aliyozungumzia ni pamoja na suala na Sahara Magharibi , na Taiwan .

Amani na usalama ni muhimu kwa dunia

Rais Assoumani amesema suala la ugfaidi bado ni tishio kubwa duniani ikiwemo katika Ukanda wa Afrika Mashariki ambako ametaja kundi la kigaidi la Al-Shabaab linaendelea kuhatarisha usalama wa eneo zima. Pia amesema makundi mengine ya kigaidi ni lazima yakomeshwe na kudhibitiwa kwa kila hali.

Hata hivyo amesisitiza kwamba “Makundi haya yanayotishia amani na usalama wa kimataifa sio Waislam , ni magaidi na hawahusiani na Uislam ambao ni dini ya amani, kuvumiliana na kuishi pamoja. Hata hivyo tunafahamu makundi haya ya kigaidi tunayopaswa kupambana nayo kuna vijana ambayo wameghubikwa na changamoto nyingi na kujikuta wametumbukia huko ndio maana natoa wito wa kuunga mkono nchi kwa mitaji ili kuwa na program za kiuchumi na maendeleo zitakazonusuru vijana hao.”

Ameongeza kuwa mshikamano wa kimataifa unahitajika kukabiliana na suala la ugaidi kwani hakuna nchi iliyo na kinga dhidi ya changamoto hiyo.

Mabadiliko ya tabianchi

Kuhusu changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ameendelea kusema nchi za visiwa vidogo vinavyoendelea kama Comoro viko hatarini endapo hatua Madhubuti hazitochukuliwa na kila nchi na hasa wachangiaji wakubwa wa uchafuzi wa mazingira. 

Amesema kila nchi iko hatarini iwe ni kwa mafuriko, vimbunga, moto wa nyika, maporomoko ya udogo na majanga mengine yanayochangiwa na mabadiliko ya tabianchi. 

Amesisitiza kuwa nchi zinazoendelea ambazo sio wachangiaji wakubwa wa mabadiliko hayo ndio wanaobeba gharama kubwa na hasa visiwa vidogo vinavyoendelea ikiwemo Comoro. 

Ametoa wito kwa dunia nzima kushikamana ili kuepusha zaiha kubwa ya janga hilo kwa kizazi cha sasa na kijacho.